Kwa mujibu wa kifungu cha 55 (1) cha sheria namba 2 ya mwaka 2007, Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ni chombo pekee chenye dhamana ya kusimamia huduma za Hijja Zanzibar.
Katika kutekeleza jukumu hilo, Kamisheni ina uwezo na wajibu wa:-
i. Kuiwakilisha Zanzibar kwenye Shughuli (forum) za Kimataifa zinazohusiana na Hijja ambazo huhudhuriwa na vyombo vyenye hadhi na sifa ya Kamisheni.
ii. Kuiwakilisha Zanzibar katika mambo yanayohusiana na Hijja ambayo Zanzibar inapaswa kuwakilishwa.
iii. Kulinda hadhi na maslahi ya Zanzibar katika mambo yote yanayohusiana na Hijja.
Katika kufanikisha dhima hiyo Kamisheni ina dhamana ya:-
a. Kuandaa na kusimamia Mipango na Shughuli za kuimarisha huduma za Hijja.
b. Kuandaa na kusimamia Kanuni na Miongozo inayotawala shughuli za Hijja.
c. Kusimamia utendaji wa Taasisi za Zanzibar zinazosafirisha mahujaji.
d. Kutoa vibali vya kusafirisha Mahujaji kwa Taasisi zilizosajiliwa kwa kuzingatia masharti na miongozo iliyopo.
e. Kuhakiki uwezo wa masheikh na wasimamizi wa misafara ya Taasisi za Hijja.
f. Kusuluhisha mizozo baina ya taasisi za Hijja; au/na kati ya taasisi za Hijja na mahujaji.
g. Kufanya tathmini kila mwaka ili kuangalia namna taasisi za Hijja zilivyotekeleza ahadi na makubaliano yao na mahujaji.
h. Kupitia kwa kina miongozo ya Hijja inayotolewa na Saudi Arabia na kuiarifu Serikali pamoja na taasisi zake ili kurahisisha utekelezaji wake.
i. Kufanya kazi za Sekretariet katika Kamati ya Hijja ya Zanzibar, Afisi Kuu ya Mambo ya Hijja Tanzania (Biitha) na Kamati nyenginezo zinazosimamia Hijja.
j. Kuratibu, kushauri, kupanga na/au kufanya maandalizi yanayohitajika kwa wajumbe rasmi wa Serikali wanapotaka kwenda safari za Hijja.
k. Kuandaa Ripoti ya Shughuli za Hijja kwa mwaka na kuiwasilisha kwa Waziri.
Kwa sasa, Kamisheni pia inaongoza Biitha ya Tanzania ambayo bado haijawekewa Muundo rasmi wala taratibu za kuiendesha. Shughuli zote zinazohusu Biitha hufanywa kwa mazowea na makubaliano yanayofikiwa ili kukidhi masharti ya kuwawezesha watanzania kutekeleza ibada ya Hijja. Shughuli hizo hufanywa kwa mashirikianao baina ya Kamisheni, Wizara ya Mambo ya Nje, Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) na Umoja wa Taasisi za Hijja Tanzania Bara (TAHAFE). Biitha ndio kiungo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Saudi Arabia katika masuala yanayohusiana na Hijja.
Miongoni mwa kazi za Biitha ni:-
a)Kuratibu na kusimamia mawasiliano yote yanayohusiana na shughuli za Hijja baina Tanzania na Saudi Arabia.
b)Kuhudhuria vikao vinavyoitishwa na Wizara ya Hijja ya Saudi Arabia kwa ajili ya kutathmini shughuli za Hijja iliyopita na kusaini makubaliano ya uendeshaji wa Hijja ijayo pamoja na kuyasimamia makubaliano hayo kwa upande wa Tanzania.
c)Kuzitambulisha Taasisi za Hijja na viongozi wake katika Mamlaka mbali mbali za Saudi Arabia zinazohusiana na Hijja.
d)Kusimamia mtandao wa kielektroniki wa Biitha unaosajili mambo yote ya Hijja, Taasisi na mahujaji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
e)Kusimamia na kutunza mali na hesabu za Benki zinazohifadhi fedha za Biitha na amana za Taasisi kwa upande wa Tanzania na Saudi Arabia.
f)Kuunda na kusimamia Kamati za utoaji wa huduma kwa Taasisi na mahujaji pamoja na kufanya mawasiliano ya kiutendaji katika maeneo yote ya Jeddah, Makka na Madina.
g)Kulinda haki na maslahi ya Taasisi na mahujaji katika mambo yanayohusiana na Hijja.
h)Kuandaa na kusimamia Taratibu na Miongozo inayohusiana na usimamizi wa Hijja.
i)Kuunganisha Taasisi zinazoandaa safari za Hijja na Umra kutoka Tanzania.
Zanzibar ina jumla ya taasisi 19 zilizoruhusiwa kupeleka Mahujaji. Taasisi zote za Zanzibar zinaunganishwa na Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) isipokuwa Ahlu Daawa. Kati ya Taasisi za Hijja ziko zenye hadhi ya Kampuni za Usafirishaji (travelling Agencies), Jumuiya za Misaada (Charitable Organisation), Jumuiya za Kidini (Faith Based Organisation) na Jumuiya za kiraia (Civil Siciety).Taasisi hizo ndizo zinazoingia mkataba wa kuuza huduma kwa mahujaji; hivyo, ndizo zenye dhamana ya kuwatekelezea mahujaji makubaliano hayo kwa kusajili na kusafirisha Mahujaji. UTAHIZA hushughulikia maendeleo ya Taasisi za Hijja na huduma za Hijja, aidha; kusawazisha migogoro baina ya wanachama na ikishindikana hupelekwa Kamisheni. Kwa maelezo zaidi ya hijja ya mwaka huu tafadhali kliki hapa.